Habari

Imewekwa: 14/11/2018

TMA kufunga RADA Mpya nne

TMA kufunga RADA Mpya nne

Katika jitihada za kuzidi kuboresha huduma za hali ya hewa nchini, Serikali ya awamu ya tano imekamilisha upatikanaji wa radar ya hali ya hewa ya tatu kwa kusaini mkataba utakaochukua miezi kumi na nne (14) mpaka kukamilika kwa radar hiyo. Radar hiyo itafungwa mkoani Mtwara, Mikindani katika kilima cha Mbae.

Akizungumza wakati wa kusainiana mkataba huo, mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Buruhani Nyenzi amesema kuwa lengo ni kuhakikisha mamlaka inazidi kujengewa uwezo wa kuendelea kuboresha huduma zake hususani katika kutoa utabiri sahihi wa hali ya hewa, hivyo upatikanaji wa radar hii ni neema kwa wananchi wa mikoa ya Kusini mwa Tanzania. Aidha aliongezea TMA iko katika hatua za mwisho za zabuni ili kukamilisha ununuzi wa radar nyingine mbili zitakazofungwa Kigoma na Mbeya.

Kwa upande wa mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi aliishukuru serikali kwa jitihada zake za kuboresha huduma za hali ya hewa nchini kwa kuendelea kukamilisha ahadi ya kufungwa radar saba nchi nzima, hii ikiwa radar ya tatu baada ya kufungwa kwa radar iliyopo Dar es Salaam na Mwanza.

Naye mwakilishi wa Entrerprise Electronics Corporation (ECC) kutoka Marekani bw. Edwin Kasanga alihakikishia bodi na menejiment ya TMA kuwa watamaliza kazi kwa wakati kulingana na makubaliano ya mkataba ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa radar ya kisasa zaidi.