Habari

Imewekwa: 19/11/2018

UZINDUZI WA TOVUTI NA LOGO

UZINDUZI WA TOVUTI NA LOGO

Kaimu Katibu Mtendaji wa NACTE Mhandisi, Dkt. Annastellah Sigwejo amekipongza Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa ‘NMTC’ kwa jitihada zake za kukitangaza chuo kitaifa na kimataifa. Pongezi hizo zilitolewa wakati wa uzinduzi wa tovuti na nembo mpya ya chuo hicho. ‘Nawapongeza kwa kuhakikisha kunakuwa na tovuti ya chuo ikiwa ni moja ya vitu ambavyo NACTE inahimiza, aidha tovuti ya chuo ni muhimu sana na ina faida kubwa kwani hukitangaza chuo kwa upana sana kitaifa na kimataifa’. Alisema Dkt. Sigwejo.

Vile vile, aliongezea kwa kusema, ‘kwa vile tovuti hii imeunganishwa na tovuti-mama ambayo ni ya Mamlaka ha Hali ya Hewa Tanzania ‘TMA’ itasaidia pia watumiaji kupata taarifa za hali ya hewa nchini ambazo ni za muhimu sana kwa wananchi kwa sekta zote za maendeleo ya nchi pamoja na wananchi kwa ujumla wake’.

Aliendelea kwa kuelezea kuwa kwa taarifa aliyonayo ni kwamba kuna vyuo viwili tu vya hali ya hewa katika ukanda wa Afrika Mashariki, hivyo kwa kupitia tovuti ya chuo, chuo kitajulikana zaidi au kitawafikia watu wengi zaidi ndani ya nchi na nje ya nchi na hivyo kuongezeka kwa udahili, muhimu ni kuhakiksha vigezo vya utoaji elimu vinafuatwa.

Uzinduzi wa tovuti (www.nmtc.ac.tz) na nembo ya chuo ulifanyika rasmi tarehe 15 Novemba 2018, katika ukumbi wa chuo cha NMTC-Kigoma na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu manispaa ya Kigoma.

Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa (National Meteorological Training Centre (NMTC) ni chuo kilicho chini ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na ni chuo pekee nchini kinachotoa taaluma ya hali ya hewa katika ngazi ya cheti (NTA-Level 5) na diploma (NTA-level 6). Chuo kimesajiliwa kwa usajili wa kuduma mwaka 2014 na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ili kutoa elimu bora yenye kukidhi viwangona kwa sasa kipo katika mchakato wa kupata ithibati (Accreditation).